“Angalia
katika nchi za kiafrika kama Kenya, wale watu huziibia nchi zao na kwenda
kuwekeza katika nchi za nje...Hawa ni watu wanaoagiza kila kitu kutoka nje mpaka
na njiti za kiberiti. Kwa mawazo yangu, nchi nyingi za kiafrika zilitakiwa
ziendelee kutawaliwa kwa miaka 100 kwa sababu hawajui lolote kuhusu utawala
bora”. ni maneno kutoka kwa Donald Trump,
bilionea linaloomba ridhaa kugombea urais wa Marekani mwakani kupitia cha chama
cha Republican. Jamaa linadharau “kinoma!”.
Kwamba sisi tunaagiza kila kitu kutoka nje hadi njiti za kiberiti. Hivi
ni kweli njiti za Kiberiti sizinatengenezwa Mufindi? Kwamba tulitakiwa
tuendelee kutawaliwa na wakoloni. Linatukumbusha
“ukuda” wa Waingereza walipotuchongea huko umoja wa Mataifa kwamba Tanganyika
haijawa tayari kujitawala labda mpaka mwaka 2059. Tumshukuru Mungu Mzee Nyerere
“alikomaa” mpaka kikaeleweka. Leo tunasherehekea miaka 52 ya Uhuru pamoja na
kwamba bado tumevaa nepi. Lakini hivi ni kwa nini? Yaani karibu nchi zote za
Afrika zimevaa nepi na uzee wote huo. Aibu! Shida ni matendo yetu. Matendo
yameyopelekea tutukanwe na tukatukanika. Nitasema tu!
Kati ya weupe wote waliowahi
kumtukana mtu mweusi, aliyevunja rekodi ni aliyekuwa mfalme wa ubaguzi wa rangi enzi hizo Afrika
Kusini, Peter Botha. Mwaka 1985 akilihutubia baraza lake la mawaziri
alitutukana eti weusi hatuna lolote jema, isipokuwa mashujaa wa kupiga kelele, kucheza
ngoma, kuoa wanawake wengi na kupenda sana ngono. Kwamba mtu mweusi ni alama ya
umaskini, udumavu wa akili, uvivu na aliyekosa ushindani”. Botha alikuwa mjinga
kweli. Yaani na ufalme wake wote alishindwa kuelewa kwamba kusema ukweli Afrika
ni dhambi! Au hata wewe unayenisoma hujui kama kusema ukweli katika nchi ambazo
viongozi huwaibia watu wao kusema ukweli ni kosa? Kama huamini muulize Mnyika
kilichompa pale aliposema kiranja wa nchi yake ni dhaifu.
Lakini pengine tabia za kucheza,
kupenda ngono na utawala wa ubabaishaji utakuwa unatuhusu. Nasema Hata Comte
Joseph – Arthur Gobineau miaka ya 1800 amewahi kuandika kwamba waafrika ni watu
wanaokosa ubunifu wa kisanyansi na kisiasa badala yake wanafaa zaidi kwa kazi
ya kucheza, kuvaa na kuimba alipata msuko. James
Watson,
mwanasayansi maarufu sana duniani na mshindi wa nishani ya Nobel katika tiba
mwaka 1962, aliwahi kusema pia mtu mweusi ana akili kidogo kuliko mtu mweupe.
Lakini swali la msingi ni kwa nini matusi hayo yaelekezwe kwa weusi tu? Unajua
ukisoma vizuri kitabu cha Chancellor Williams, “Destruction of Black
Civilization: Great Issues of a Race from 4500 B.C. to 2000 A.D” utagundua
weusi ndo tulikuwa mbele kwa kila kitu. Tulifanya mambo makubwa sana
yaliyothibitisha kwamba uwezo wetu wa kufikiri ulikuwa juu. Je tulipotea wapi? Kwa
sababu haiwezekani watu mashuhuri wautilie shaka uwezo wetu wa kufikiri.
Siku
za nyuma mawaziri kadhaa waJapan walipata kusema kwamba wanatilia shaka uwezo
wa mtu mweusi katika kufikiri. Yaani huyu pamoja na kwamba weusi tunashindana
kununua magari ya Japani na bidhaa nyingine bado anatilia shaka uwezo wetu wa
kufikiri? Au ni hayo magari ya bei mbaya tunayoshindana kuwanunulia viongozi
wetu na wakati viongozi wetu hawaishi kupigana vikumbo huko ughaibuni kuomba
omba? Chika Onyeani katika kitabu chake cha Capitalist Nigger naye anashangaa ni kwa nini Mwafrika
atukanwe namna hiyo na mawaziri wa Japan lakini bado waendelee kununua bidhaa
toka Japan. Chika alitegemea tungesusia mabidhaa ya kutoka Japan.
Sidhani
kama kususia bidhaa inatosha na badala yake tuyatathimini matendo yetu.
Tubadilishe tunavyoenenda. Tuache kwenda kama Tumbiri. Manyanyaso,matusi na kila aina ya dharau
vitaisha pale tu tutakapo jitambua, kujiheshimu na kujikubali. Kwa nini nasema hivyo? Tumevunja rekodi katika
kutafuta ufahari wa kijinga na kusahau mambo ya maana. Profesa Ali Mazrui amewahi
kuandika, “Mwafrika hawezi kuwa mshiriki
mzuri katika ubinafsishaji kwa sababu hana utashi na ari ya kupata faida na
ulimbikizaji badala yake anatawaliwa na majivuno na ufahari; ni
mfanyabiashara mbaya asiyeweza kutegemewa”.Yaani tunaona fahari
kwenda kuombaomba na kujidhalilisha mbele ya wazungu na wakati tunakila kitu.
Hata wao wanachoshwa na tabia zetu za ombaomba. Jenerali Ulimwengu amewahi
kuandika kwamba kinachowaudhi wazungu
zaidi ni tabia yetu ya kuombaomba inayoambatana na ubadhirifu wa kutisha.
Hawaelewi ni jinsi gani nchi inaweza kutembea kote duniani ikiombaomba kwa
kusafiri daraja la kwanza wakati wafadhili wenyewe wanasafiri daraja la
kawaida. Ni kama ombaomba uliyemtupia shilingi mia tano hapo mapema umkute
hotelini anafurahia ‘lobster’ na mvinyo. Ulimwengu huwa anamaneno!
Ukweli ni kwamba tunafanya upuuzi
kwa sababu wazungu wametutikisa kidogo tukanywea, tukajiona sisi kweli ni
washenzi na ishara ya laana na umaskini. Tukajikuta tunamtukuza mzungu. Leo hii
mtu mzima anaona ustarabu ni kuwa na rafiki mzungu, kuishi ulaya na kufanana na
mzungu. Hiyo ndiyo definition ya maisha tuliyonayo. Carter G. Woodson katika kitabu chake
kiitwacho, “Miseducation of the Negro” anasema, “If
you can control a man’s thinking you do not have to worry about his action.
When you determine what a man shall think you do not have to concern yourself
about what he will do. If you make a man feel that he is inferior, you do not
have to compel him to accept an inferior status, for he will seek it himself”. Wazungu
wametufanya washenzi nasi tukakubali na kwa nguvu zote tukawekeza katika
kujikana wenyewe na kuwa wazungu. Hakuna anayekulazimisha kujichubua, hakuna
anayekulazimisha kuvaa manyoya kichwani, hakuna anyekulazimisha kuongea kama
wazungu. Utajikuta unafanya mwenyewe, tena kwa gharama za juu. Woodson anakwambia, “If
you make a man think that he is justly an outcast, you do not have to order him
to the back door. He will go without being told; and if there is no back door,
his very nature will demand one and cut one to enter”.Hiyo ndiyo siri pekee
anayoitumia mtu mweupe kumshenzisha mtu mweusi.
Leo
hii hata ukijaribu kuongea Lugha yako ya asili lazima utachekwa tu na pale
utakapoogea Lugha ya Mzungu utasifiwa na kila mtu. Lugha zetu za asili
tunaziita vernacular languages.
Jamaa yangu mmoja amekata channels zote za kizungu kwenye luninga yake na
kununua katuni zinazozungumza kizungu tu kwa lengo la kwamba watoto wake
waongee kizungu. Matokeo yake watoto wanakula kama katuni, wanacheza kama
katuna na kuongea kama katuni. Pale nyumbani hawasikilizani. Sasa kwa mwendo
huu tukiitwa tumbiri wanaozungumza tutamlaumu nani?
Matusi haya siyo ya bure, ni kwa
sababu ya mienendo yetu. Sisi pamoja na usomi wetu bado tu hamnazo. Yaani kila
elimu inavyozidi kuongezeka ndivyo mtu mweusi anavyozidi kujikataa. Angalia
wasomi wote, wanashangaza. Pengine ndiyo maana inasemekana “ Ni rahisi sana kumtawala msomi wa Kiafrika kuliko Mwafrika asiye na
kisomo, kwa sababu Mwafrika asiye na kisomo anamwamini sana ndugu yake
aliyesoma”. Kujikataa kote huku kumeletwa na wasomi. Jenerali Ulimwengu anasema,
“Tunauchukia Uafrika, na ingekuwa inawezekana tukaumbwa upya katika muonekano
mwingine, bila shaka tungeteua kuwa Wazungu au Waasia, au Waeskimo, kwa jinsi
tunavyoona dada zetu – wakati mwingine hata wanaume – wakijichubua ili wawe na
ngozi nyeupe. Leo hii, zaidi ya nusu ya wanawake unaokutana nao wamefunga
manyoya kichwani yanayofanana na nywele za Kizungu au Kiasia. Manyoya haya,
ambayo ni ya gharama kubwa, yananunuliwa hata na wanawake ambao hawajui mlo
ujao utatoka wapi, lakini fasheni ni kuwa Mzungu bandia, na hilo ni muhimu
kuliko chakula”.
Yaani ukiisha ikamata akili ya
mwanadamu huna haja ya kutumia nguvu nyingi kumuelekeza kujikataa. Ulimwengu
anaendelea kuzungumza kupitia maandisha yake, “Tumeambiwa mara kwa mara kwamba
kuchubua ngozi ni hatari kwa afya yako kwani kunasababisha ngozi iathirike na
mionzi ya jua, na hilo linaweza kusababisha saratani, lakini hatusikii, kwa
kuwa labda ni bora uwe Mzungu kwa muda mfupi halafu ufe kuliko kuishi miaka
mingi bila kuwa Mzungu walau kidogo. Manyoya yanayovaliwa na akina mama wakati
mwingine huja yakiwa yamebeba chawa na minyoo, na ni rahisi kwa wadudu hawa
kuwaumiza wavaaji wa manyoya hayo”. Ndiyo maana Malcom X anakuuliza, “Who taught you to hate the
texture of your hair? Who taught you to hate the color of your skin? To such
extent you bleach, to get like the white man. Who taught you to hate the shape
of your nose and the shape of your lips? Who taught you to hate yourself from
the top of your head to the soles of your feet? Who taught you to hate your own
kind? Who taught you to hate the race that you belong to so much so that you
don't want to be around each other?”.
Wazungu wanatuangalia na
wanatufuatilia katika kila tunalofanya, na kwa kuwa wanajua kwamba
tunajidharau, nao hawana la kufanya ila kutudharau. Walitwambia kwamba ili
tuinue uchumi wetu tunatakiwa kuondoa ruzuku na tukakubali. Wakati
ng’ombe mmoja wa Ulaya analipwa ruzuku ya dola za Marekani kwa siku, huku
kwetu wafugaji ndiyo wamekuwa mitaji ya maafisa mifugo. Kila akimchoma ng’ombe
wako sindano ya chanjo lazima umlipe.
Sasa ukihesabu gharama za ufugaji lazima uachane na shughuli hiyo. Erik Reinert kupitia kitabu chake, “How Rich
Countries Got Rich . . . and Why Poor Countries Stay Poor” anatoa ushauri kwa
nchi maskini kwamba zisifanye kile ambcho nchi tajiri wanasema, bali wafanye
kile nchi tajiri wanachofanya. Pamoja na ushauri wote huo bado tunaendelea
kuiishi kwa za kuambiwa.
Kujitoa
kwetu ufahamu kumeendelea kutufanya tuamini uzungu ndiyo mwarobaini wa
mafanikio. Ilifikia kipindi kiranja mkuu wetu na washabaki wa mpira wa miguu
kuamini kocha wa kizungu ndiyo atamaliza matatizo ya mpira ili tukawafunge
Brazili. Utasikia, “Leta
kocha wa kizungu, waweke vijana kambini, wapate msosi freshi, vijana watanoleka
bila taabu, kisha tunakwenda kucheza Kombe la Dunia”. Hivi kwa mtindo huu
tukiitwa tumbiri wanaoongea tutachukia? Kwa
mawazo mafupi namna hii kama mkia wa mbuzi mataifa
makubwa, yataendelea kutuita washenzi, ma-mbumbumbu, hohehahe wasio na nyuma
wala mbele.
Historia inaonyesha kwamba chuo kikuu cha kwanza duniani
kilikuwa Afrika, kule Mali. Maajabu mengi yaliyofanyika Misri, yalifanywa na
Weusi. Uvumbuzi wa hisabati ulitoka Afrika, hata mtu wa kwanza duniani
anaaminika kuishi Afrika. Hata Yesu alikuwa mweusi! Mapapa watatu wa mwanzo
kabisa walikuwa weusi. Hata Yesu Kristu, alikuwa Mweusi wa Misri, na ndiyo
maana Simon wa Krene, ambaye kwenye Injili, tunaambiwa alikuwa Mweusi
alimsaidia Yesu, kubeba msalaba. Ilikuwa ni huruma ya kuona Mweusi mwenzake
anateswa ameandika Padri Karugendo, mwandishi nguli katika Makala kwenye gazeti
la Rai Mwema. Lakini Aylmer Von Fleischer (How Jesus Christ Became
White) anaandika, “One of the major
reasons why the image of Jesus Christ was changed from Black to White was
because of the rise of White supremacy in Europe and across the world, and the
demise of the Black race. Whites were heavily involved in the destruction of
many Black civilizations like the Indus, ancient Egyptian and Hebrew"
Na baada ya hapo weusi wakaufananisha shetani. Hata ukiangalia katika vitabu
vyao vyote shetani ni mweusi. Hiyo ni
danganya toto. Lakini
chukua muda, soma kitabu cha, “ The
Destruction of Black Civilization” kinapatikana kwenye mtandao tena kwa bure.
Akiongea na weusi wenzake Bill Cosby
aliwahi kusema, “Men, if you want to
win, we can win,” . “We are not a pitiful
race of people. We are a bright race, who can move with the best. But we are in
a new time, where people are behaving in abnormal ways and calling it normal”. Kuzikataa nywele zako na kuvaa za mzungi
ni kubehave in abnormal ways and calling it normal, kuikataa rangi yako na
kujichubua kuwa kama ya mzungu ni kubehave abnormal
ways and calling it normal, kutamani kuishi kama mbwa Ulaya ni kubehave in abnormal ways and calling it normal,
kuwalazimisha watoto wako kuikataa lugha ya mababu zako ni kubehave in abnormal
ways and calling it normal. Tubadilike. Tuache ukenge, maisha yanawezekana
hapa hapa nyumbani. Unachotakiwa
ni kubadilisha namna ya kufikiri tu. Naamni ukisoma vizuri kitabu changu cha
Ukombozi wa Fikra utajikubali na kuifurahia Dunia. Tukibadilika mazuri yatatoka
kwetu kama asemavyo Patrice Lumumba
katika barua yake ya mwisho kwa mkewe, Pauline “Siku moja Historia itajieleza; haitakuwa Historia inayotolewa Umoja wa
Mataifa, Washington, Paris wala Brussels, bali ni Historia ya Afrika. Siku moja
Afrika itaandika Historia yake yenyewe, Kusini na Kaskazini mwa Jangwa la
Sahara kutatukuka.”
Tukiruhusu akili zetu kufanya kazi kwa
kudadisi, kuhoji na kufikiri kwa kina siku moja magazeti ya Tanzania
yataandika, “Tanzania
itasitisha misaada yake kwa Marekani
kutokana na vitendo vya ubaguzi nchini humo”, “ India yashukuru msaada
kutoka Tanzania ambao ulipanga kuwasaidia wahanga wa mafuriko ambayo
inasemekana hayajawahi kutokea tangu
uumbwaji wa dunia”, Uingereza yaandaa mapokezi makubwa kumpokea Mhe, Rais
kutoka Tanzania. Siyo utani, ni
ukweli tu. Wazungu waliweza kuvuruga ustaraabu wa mtu mweusi kwa kucheza na
akili tu. Akili ni injini ya mwili, pale inaponoki gari halisongi. Njia pekee
ya kujifunza kufikiri ni kufikiri, kudadisi ni kudadisi na kuhoji ni kuhoji.
Kazi ya kichwa siyo kufuga nywele ni kufikiri vizuri. Tukibadili namna ya kufikiri,
tukajenga utamaduni wa kuhoji na kudadisi naapa Tanzania itakuwa na watawala
wanaoendesha nchi yetu katika misingi ya
akili na mantiki, ikiwa na viwanda vya kutengeneza bidhaa badala ya kuuza
mali-ghafi. Tutaacha kusafirisha ajira za vijana wetu kwenda China na
mali-ghafi zetu zitatumika kuzalisha ajira hapa hapa Tanzania
kwa ajili ya vijana wetu. Tutakuwa nchi ya viwanda, utafiti, uvumbuzi,
usomi uliotukuka, na falsafa ya kina. Tutaondokana na njaa, maradhi na
umasikini katikati ya neema kubwa. Watu wetu wataishi maisha ya staha na
furaha. Watoto wetu, wanawake wazazi na wazee watakuwa na siha bora maisha yao
yote.
Tukifikia hatua vijana wa kizungu
watatuheshimu kwa sababu tutajulikana kama watu makini, watu wenye mantiki,
siyo ombaomba. Watakuja kujifunza kutoka kwetu kwa sababu tutakuwa tunafanya
maajabu. Watatamani kuwa weusi. Watabadili hata nywele zao kuwa kama zetu. Tujenge
utamaduni wa kuhoji kwa kila kitu ili tusiwe kama waziri mmoja wa Tanzania waziri
mhusika wa sekta ya madini alitembelea machimbo ya dhahabu, akapitishwa sehemu
kadhaa, lakini alipotaka kuingia chumba cha kuhifadhia dhahabu akazuiwa kwa
sababu za ‘kiusalama na bila hata kuhoji alifyata mkia. Jamani kutohoji hukufanya ufyate
mkia.
Mshairi Marcelino Dos
Santos wa Msumbiji anasema; "We Must Plant". Kwa maana ya tuna
lazima ya kupanda. Dos Santos hazungumzii kupanda mbegu za mahindi au mtama,
bali kupanda fikra za makini kwa wanajamii. Fikra zitakazowasaidia kutoka
katika hali iliyopo na kwenda kwenye hali nyingine iliyo bora zaidi.