Jumamosi, 26 Desemba 2015

Tunahitaji Ukombozi wa Fikra

Mara baada ya kupata uhuru wa bendera, Mwl Julius Nyerere alielekeza nguvu katika ukombozi wa fikra. Mwalimu aliamini bila ukombozi wa fikra, watanzania wataendelea kuishi utumwani. Kwa hiyo alitumia elimu kupambana na utumwa wa fikra. Alipeleka vijana wengi karibu kila kona ya dunia kuitafuta elimu. Lakini kwa bahati mbaya wengi wakaenda kupambana na mitihani badala ya utumwa wa fikra. Wakarudi na vyeti bila fikra za kimaendeleo na wakageuka kuwa tishio kwa rasilimali zetu. Kwa ujumla juhudi zake za kutukomboa kifikra zikawa zimegonga mwamba. Mpaka anaiaga dunia Nyerere katuachia uhuru wa bendera tu. Uhuru ambao mwenye nacho ndiyo binadamu na asiyenacho ni taka taka. Machinga jijini Mwanza na Dar es Salaam wanaitwa taka taka. Ndiyo uhuru huo tunaojivunia watanzania. Uhuru unao wagawa watu kwa kipato na si utu. Huu siyo uhuru, ni hatua ya kwanza katika ukombozi. Hatua ya pili ni ukombozi wa fikra na ukombozi wa kiuchumi ndiyo hatua ya mwisho.

Kitendo cha kupiga deki barabarani ili wanyonyaji wapite ni ishara ya kwamba bado tu watumwa wa fikra. Kuzunguka dunia nzima kuleta wawekezaji wasiokuwa na mitaji ni utumwa wa fikra. Kuwarudisha madarakani wezi wa rasilimali zetu huku hatuna huduma za jamii ni udumavu wa fikra. Kumshangilia jamaa anayefanya uwe hivyo ulivyo leo kwa sababu tu kakupatia tsheti, kofia na pombe kidogo ni ishara ya kwamba akili zetu haziko sawa sawa. Aliyesema umaskini wa watanzania uko kichwani kwakweri hajakosea. Maajabu tunayoyafanya yanathibitisha hivyo.  Wapare wanakwambia ni heri kuchakaza nguo kuliko kuchakaza akili. Akili ikichakaa lazima utavunja rekodi katika kufanya maajabu.  Leo hii tunawalamba miguu wezi wa rasilimali zetu. Hivi kama haya siyo maajabu ni nini? Kucheka na mtu aliyesababisha hospitali zikose dawa, watoto wako wafukuzwe shule kwa kukosa ada, mazao yako kukosa soko na biashara yako kukosa faida ni uthibitisho wa wazi kwamba tuko huru gereni. Wallahi tumerogwa. Siyo bure.Haiwezekani uendelee kumsujudia mtu aliyekula hela yako ya likizo tukasema uko salama kichwani, tutakuwa tunakuonea. Unahitaji tiba! Yaani ukombozi wa fikra ili uweze kuona mambo katika uhalisia wake.

Kwa mfano, watawala dhalimu pamoja na kutukalia kichwani bado tunawapa ridhaa ya kurudi madarakani na kuwaacha wale viongozi wazuri. Haiwezekani aliyepinga ubadhirifu wa ESCROW anyimwe ubunge na wakati aliyepiga arudi bungeni kwa kishindo halafu tuseme sisi siyo wagonjwa. Tunaumwa Stockholm.  Stockholm ni ugonjwa wa kumpenda na kumtetea adui yako. Ndiyo maana nasema Nyerere aliondoka hajaimaliza kazi ya kutukomboa kifikra. Lakini kuondoka kwa Nyerere isiwe kigezo cha sisi kushindwa kuutafuta ukombozi wa fikra. Tuendelee kupamba na utumwa huo, vinginevyo tutaendelea kuogelea kwenye umaskini endelevu.  Denis Waitley aliwahi kusema,  “Maisha siku zote yamejaa hatari tu. Lakini kunahatari moja kubwa ambayo unatakiwa kuizuia kwa gharama yoyote na hiyo ni hatari ya kutofanya lolote”.Kuendelea kujitoa ufahamu kwa kuwakumbatia mafisadi ili waendelee kutafuna keki ya taifa hili ni hatari ya kutofanya lolote katika maisha yetu. Ndiyo maana nasema tunahitaji fikra ya kuweza kuyaona . Kuendelea kucheka na nyani tutavuna mabua.

Tunahitaji kuamka na kusema kutumika sasa basi. Urafiki gani wa siku za uchaguzi na kuwa taka taka baada ya uchaguzi? Hii danganya toto ya kwamba machinga ni rafiki wa watawala wakati wa kampeni ni matusi na kumbuka   akutukanaye hakuchagulii tusi. Kama huamini ninacho kisema, angalia inapokaribia uchaguzi machinga wanakuwa rafiki wa serikali. Wanauza bidhaa zao kiholela, yaani kila palipo na upenyo wapo. Baada ya uchaguzi wanageuka kuwa takataka ambazo mwisho wa siku lazima ziondoke. Atakayekaidi lazima akutane na askari mgambo. Yaani ndugu zangu askari mgambo ndo hawajitambui kabisa. Kwa posho ya shilingi 5000 yuko tayari kumpiga mlalahoi mwenzao. Jamani hata kuelewa hili tunahitaji kuwa na elimu ya chuo kikuu? Hapa ni ukombozi wa fikra tu.  

Watanzania tuko huru lakini uhuru wa bendera hautoshi. Uhuru wa bendera haufai hata kidogo. Uhuru wa bendera ni sawa na kuvaa suruali isiyo na zipo ukweni, utakuwa mtu mwenye wasiwasi, mashaka na aibu. Uhuru wa bendera umetujengea wasiwasi, na nidhamu ya woga na mwisho wa siku watawala dhalimu kuendelea kutunyonya kutokana na wasi wasi wetu. Kama ilivyo kwa  uhai wa samaki kwenye maji ndio ilivyo uhuru wa bendera kwa uhai wa wanyonyaji.  

Ndiyo maana tunahitaji kuutafuta ukombozi wa fikra na mengine tutazidishiwa. Tuhakikishe kichwani panakuwa vizuri. Kichwani pakiwa vizuri hutakuwa na haja ya kukimbizana na samaki bwawani kama unataka kuwatokomeza. Badala yake ni kuwakaushia maji yote na hapo utawakamata kirahisi sana. David J. Schwartz kupitia kitabu chake cha, “The Magic of Thinking Big” anasema, “fikra zinazoongoza akili yako ni muhimu zaidi ya kiasi cha akili ulizo nazo”.

Fikra sahihihi zinahitaji utulivu wa akili. Fikra sahihi hazihitaji papara. Kuwa na muda wa kufikiria ndilo chimbuko la uvumbuzi na maendeleo yote duniani. Maendeleo hayawezekani bila mabadiliko ya fikra na wale ambao hawawezi kubadili namna wanavyofikiri hawawezi kubadili chochote, alisema George Bernard Shaw. Tunahitaji kufikiri kwa usahihi kwa kila tunalolifanya. Tunahitaji kuwa na karakana za kufikiri akilini. Kama hulitaki jambo fulani libadilishe, kama huwezi kulibadilisha badili unavyofikiria juu ya jambo hilo alisema Mary Eugebreit. Badala ya kufikiri umaskini tulionao ni mapenzi ya Mungu tufikiri umaskini kama matokeo ya uzembe wetu. Mungu  ametupa rasilimali nyingi ambazo kama zingelitumika kwa faida yetu, zingeliweza zikatuinua tukawa matajiri. Tufikiri kwanza ndipo tutende. Kwame Nkrumah alisema, “matendo pasipo mawazo ni upofu, mawazo pasipo vitendo ni utupu”. Tunapo waachia watu wengine  madini kila kona ya Tanzania bila kuchangia vya kutosha katika maendeleo ya nchi hii ni utupu na upofu. Mungu aliyaweka madini haya nchini kwetu ili tuweze kujitajirisha na kutokomeza umasikini.

Nimalizie kwa kuwaasa watanzania wenzangu kwamba, saa ya ukombozi wa fikra ni sasa. Tusitegemee kama kuna mtu atakuja kutukomboa isipokuwa ni sisi wenyewe alisema Bob Marley, katika wimbo wake , “Redemption”. Bila fikra huru tutaendelea kushuhudia watawala dhalimu wakishindana katika matanuzi. Akinunua BWM, mwenzake ananunua Benz,sisi walala hoi tukiendelea kushughulikiwa vizuri na umaskini. Hii ndiyo itikadi ya Bongo. Inatia uchungu kwa nchi iliyokuwa nchi. Kumbuka laana au dhambi haikupi muda. Unakosa inakuadhibu pale pale. Gharama ya utumwa wa fikra ni kubwa. Tunakula adhabu kila siku. James Allen anasema, “Leo upo pale ambapo mawazo yako yamekuleta; kesho utakuwa pale ambapo mawazo yako yatakupeleka.” Mtu anavyofikiria katika akili yake anakuwa hivyo, na anavyochagua anakuwa hivyo”. Fikra finyu ni adui wa ndani.Tupambane nazo.   


Jiongezee maarifa kwa kusoma kitabu hiki na hakika utakombolewa kifikra. Mfalme Suleiman alisema, “ mtu mpumbavu ni yule asiyeona raha katika kutafuta maarifa, lakini daima ni mtu wa kuelezea mawazo yake binafsi. Akili ya mtu mwerevu hutafuta maarifa na sikio la mtu mwenye busara hutafuta kusikia maarifa. Mtu mpumbavu hufikiri njia yake ni sahihi daima, lakini mwenye busara hutafuta ushauri”.